1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiSudan Kusini

Rais Salva Kiir amfuta kazi waziri wake wa fedha

16 Machi 2024

Salva Kiir amemfuta kazi waziri wake wa fedha bila ya kutoa sababu, ingawa hatua hiyo imechukuliwa huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei na kushuka kwa kasi thamani ya fedha za nchi hiyo dhidi ya dola ya Marekani.

https://p.dw.com/p/4dnun
Salva Kiir Mayardit | Rais wa Sudan Kusini
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Kufukuzwa kwa waziri, Bak Barnaba Chol, kulitangazwa katika televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Pauni ya Sudan Kusini ilipoteza karibu nusu ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani hali iliyochochea kupanda kwa bei ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.

Soma pia:  Wabunge Sudan Kusini wamshutumu Kiir kukiuka makubaliano ya amani

Chol, mwenye umri wa miaka 43, na mshirika wa Rais Salva Kiir, aliteuliwa kuwa waziri wa fedha mwezi Agosti mwaka uliopita na alifanya mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuondoa majina ya wafanyakazi hewa katika daftari la serikali na pia kuziba njia za kuvujisha mapato ya serikali.

Rais Kiir amemteua Awow Daniel Chuong, waziri wa zamani wa mafuta ya petroli, kuwa waziri mpya wa fedha.

Kadiri mzozo wa uchumi wa nchini Sudan Kusini unavyozidi kuongezeka, baadhi ya watumishi wa umma hawajapata mishahara kwa muda wa miezi sita sasa.